Mwimbaji mashuhuri Sudan Kusini Vivian Nyachan amefariki

Kulingana na familia yake, mwimbaji huyo alifariki akipokea matibabu katika kituo kimoja cha afya Jijini Juba, Jumanne jioni.

Tom Mathinji
1 Min Read
Mwimbaji mashuhuri nchini Sudan kusini Vivian Nyachan, amefariki.

Mwimbaji mashuhuri wa Sudan Kusini Vivian Nyachan, anayefahamika sana kwa nyimbo za kuleta amani, amefariki baada ya kuugua kwa muda mfupi.

Kulingana na familia yake, mwimbaji huyo alifariki akipokea matibabu katika kituo kimoja cha afya Jijini Juba, Jumanne jioni.

Nyachan, ambaye anatoka jimbo la Upper Nile, aliimba nyimbo zilizopigia debe amani na mshikamano wa kijamii, ambazo zilichezwa mara kwa mara katika vituo vya redio vya kijamii na katika hafla za kitamaduni kote nchini humo.

Aidha, alijulikana sana kutokana na wimbo wake “Look at Me,” ulioenea sana nyakati za machafuko na ulihusishwa na miito ya kususia vita na ulinzi wa wananchi, wakiwemo wanawake, watoto, wakulima na wavuvi.

Nyimbo zake aliziimba kwa lugha ya Chollo (Shilluk) pamoja na kiarabu kwa mtindo wa kitamaduni.

Baadhi ya nyimbo zake zilizopendwa sana nchini Sudan Kusini na ughaibuni ni pamoja na “Wadakona,” “Amara,” “Raj Piny” na “Hakuma Ta Mara”.

Familia yake imesema kuwa siku ya mazishi yake itatangazwa baadaye.

Share This Article