Mwigizaji alazwa hospitalini baada ya kupigwa kazini

Mwigizaji huyo wa Nollywood amelazwa hospitalini baada ya kupigwa teke kifuani na mwenzake.

Marion Bosire
2 Min Read
Godwin Nnadiekwe

Mwigizaji wa filamu za Nigeria almaarufu Nollywood aitwaye Godwin Nnadiekwe amelazwa hospitalini akisemekana kuvuja damu kwa ndani baada ya kupigwa na mwigizaji mwenza walipokuwa wakiendelea kuandaa filamu.

Inaripotiwa kwamba teke hiyo ya juu kwa juu aliyorushiwa na Zubby Micheal haikuwa imeratibiwa kwenye mswada wa filamu waliyokuwa wakiandaa.

Katika chapisho kwenye Instagram Godwin alielezea kwamba alipigwa teke kali kifuani na Zubby wakiwa katika eneo la maandalizi ya filamu.

Hakutaja jina la mhusika kwenye chapisho hilo huku akisisitiza kwamba nia yake sio kuzomea yeyote lakini video aliyochapisha mitandaoni inaonyesha tukio hilo na Zubby anatambulika vyema.

Zubby Micheal alishuka gari akiwa amekasirika akaruka uzio mfupi wa chuma uliokuwepo mbele ya nyumba waliyokuwa wakitumia akaruka tena na kumpiga Nnadiekwe kifuani.

Baada ya hapo, Zubby aliingia kwenye nyumba hiyo.

Zubby Michael

Nnadiekwe alielezea kwamba hata ingawa tukio walilokuwa wakirekodi lilikuwa la makabiliano, teke kali namna hiyo haikuwa imeratibiwa.

Mwigizaji huyo alisema pia kwamba alijipeleka hospitali yeye mwenyewe na hakupokea msaada wowote kutoka kwa kampuni inayohusika na filamu aliyokuwa akiigiza.

Kufuatia kilichomkuta, Nnadiekwe sasa anaomba wahusika wa tasnia ya filamu wawe wakiangazia pakubwa usalama hasa katika mazingira ambapo kampuni za kuandaa filamu hazina bima, usaidizi wa kimatibabu au vifaa vya kujikinga.

Baada yake kuchapisha taarifa hizi, usimamizi wake pia ulitoa taarifa ukielezea kwamba hali yake ilizidi kuwa mbaya na alikuwa anavuja damu kwa ndani.

Website |  + posts
Share This Article