Waigizaji tajika wa filamu za Nigeria tasnia iliyopatiwa jina la Nollywood Patience Ozokwor, Kanayo .O. Kanayo na Ramsey Noah wametambuliwa nchini Uganda kwa kazi zao.
Watatu hao walialikwa kwa tuzo za mwaka huu za filamu na televisheni nchini Uganda za Ikon ambapo Ozokwor na Kanayo walituzwa.
Awamu ya mwaka huu wa 2025 ya tuzo hizo za Ikon iliandaliwa katika hoteli ya Serena jijini Kampala usiku wa Jumamosi Machi 29, 2025.
Ijumaa Machi 28, 2025, waandalizi wa tuzo hizo waliandaa kikao cha kubadilishana maarifa katika makao makuu ya shirika la Reach A Hand Uganda, katika eneo la Lugujja jijini Kampala.
Katika kikao hicho cha Ijumaa, Kanayo alifichua siri ya mafanikio ya tasnia ya filamu nchini Nigeria. Alisema kwamba wanatoa hadithi zao wenyewe wakilenga watu wao kwa lugha ambayo wanaelewa.
“Hiyo ndiyo sababu wanatizama kazi zetu na hiyo ndiyo historia ya Nollywood.” alisema Kanayo katika kikao hicho.
Wadau wa sekta ya filamu waliokuwepo waliangazia ufanisi na changamoto wanazokumbana nazo katika masimulizi ya hadithi ya Afrika.
Wengi walilalama kuhusu jinsi hadithi za Afrika zinasimuliwa na watu wengine ulimwenguni huku wahusika wenyewe wakitengwa.
Waliafikiana kwamba sasa wakati umewadia wa kudai tena hadithi za Afrika na kuongoza katika mazimulizi.