Bodi ya Dawa na Sumu (PPB), imewaonya Wakenya kuhusu kuwepo kwa dawa bandia ya kuzuia mimba aina ya P2 kwenye soko la hapa nchini.
Bodi hiyo imedokeza kuwa aina hiyo ya P2 ya Levonorgestrel 0.75mg, ina nambari za usajili T34197R na inasingiziwa imetenegezwa na kampuni ya Gedeon Richter Plc.
Kulingana na bodi hiyo, dawa hiyo bandia iligunduliwa baada ya uchunguzi wake katika maduka tofauti, uliobainisha tofauti kati ya dawa hiyo bandia na ile halali kutoka kampuni ya Gedeon Richter.
Tofauti hizo ni pamoja na uchapishaji wa nambari za usajili, makosa ya uchapishaji kwenye taarifa za watumizi, na mbinu ya upakiaji.
PPB , pia ilitilia shaka rangi ya manjano kwenye jina la dawa hiyo, huku nembo yake ikitumia maandishi tofauti.
“Hayo yanaashiria kuwa dawa hiyo ni bandia na haijatengenezwa na au kusambazwa na kampuni ya Gedeon Richter,” ilisema PPB.