Jaji Mkuu Martha Koome ametoa heshima ya kipekee kwa vizazi vya wanawake wa Kenya ambao ujasiri, uongozi na ulezi wao vimechangia kubadilisha taasisi za nchi na kuhamasisha viongozi wa siku zijazo.
Koome amefanya hivyo kwa kuandika kitabu kiitwacho ‘Distinguished Women Leaders: Profiles in Courage and Service Leadership in Nation Building’.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kitabu hicho kilichohaririwa na Joe Kilonzo, Koome alisema chapisho hilo ni namna ya kuwasherehekea wanawake walioijenga Kenya kupitia huduma, ustahimilivu na kujitolea kwa dhati.
Jaji Mkuu huyo akikumbuka safari yake ya kuwa mwanamke wa kwanza kuwahi kushikilia wadhifa wa Jaji Mkuu nchini Kenya, Koome alisema mafanikio yake yaliwezekana kutokana na wanawake waliotangulia, waliothubutu kupinga mila zilizowazuia, kuvunja vikwazo na kufungua fursa kwa wengine.
Alisifia wanawake walioangaziwa katika kitabu hicho kwa mchango wao katika sekta ya mahakama, biashara, elimu, utumishi wa umma na uongozi wa jamii.
Koome alisema wengi wa wanawake hao walikuwa waanzilishi katika nyanja zao, lakini hawakupanda ngazi za uongozi peke yao. Badala yake, waliwalea, kuwaongoza na kuwasaidia wengine kufikia mafanikio.
Alisema kipimo halisi cha uongozi ni uwezo wa kuwawezesha wengine kufanikiwa.
Jaji Mkuu aliwataka Wakenya kutunza na kuenzi simulizi za wanawake ambao mchango wao mara nyingi haujatambuliwa, huku akisisitiza kuwa hakuna mwanamke anayekuwa wa kwanza anayepaswa kubaki kuwa wa pekee.