Waziri wa usalama wa ndani Kipchumba Murkomen, ametetea mkataba wa maendeleo ya kitaifa uliopendekezwa na Rais William Ruto.
Anasema utatoa mwongozo wa muda mrefu wa kuleta mageuzi ya kiuchumi na kujenga mustakabali wenye heshima zaidi kwa Wakenya.
Akizungumza mjini Tot, Kaunti ya Elgeyo Marakwet, Murkomen alisema kuwa mfumo wa maendeleo utakaofuata ruwaza ya mwaka 2030 unaweka maendeleo endelevu kuwa kiini cha ajenda ya serikali.
Waziri huyo alisema kuwa Rais Ruto anaendelea kujitolea kutekeleza ajenda yake ya maendeleo kupitia uwekezaji unaoboresha maisha ya wananchi na kuchochea ukuaji wa uchumi unaowajumuisha wote.
Murkomen alipuuza ukosoaji kutoka kwa viongozi wa upinzani kuhusu mkataba huo uliopendekezwa, akiwatuhumu kwa kukosa ajenda mbadala ya maendeleo kwa taifa.
Katibu huyo aliwahimiza Wakenya kushiriki kikamilifu katika mchakato wa ushirikishwaji wa umma mara tu utakapozinduliwa, akisema maoni yao yatasaidia kuunda mfumo huo kuwa mwongozo wa kitaifa wa maendeleo unaoakisi matarajio ya wananchi wote.
Katika hotuba yake kwa taifa Julai 30, 2026, Rais William Ruto alipendekeza ruwaza ya mwaka 2060 aliyoitaja kuwa mkataba wa kitaifa wa maendeleo akisema ni mwongozo wa kikatiba.
Lengo lake kuu alisema ni kuipa mipango ya maendeleo ya taifa msingi wa kisheria ndani ya Katiba ya Kenya ya mwaka 2010.
Mabadiliko hayo ya kimuundo yanalenga kulinda malengo ya maendeleo ya uchumi wa taifa dhidi ya mabadiliko ya vipaumbele, ilani za kisiasa na maslahi yanayobadilika.