Mumewe mwanamuziki Nadia Mukami Arrow Boy jana alimwomba msamaha jukwaani kwenye tamasha ya Nadia ya kuadhimisha miaka 10 katika tasnia ya muziki.
Arrow ambaye pia ni mwanamuziki aliibuka bila kutarajiwa katika hafla hiyo akiwa amembeba mwanao wa kwanza Kai, na ghafla ikageuka ikawa kujaribu kuwaunganisha wapenzi hao.
Waliimba pamoja wimbo wao Radio Love, waliorekodi wakati uhusiano wao ulikuwa katika hali nzuri huku umati ukishangilia wengi wakifoka maneno ya kuhimiza wawili hao warudiane.
Mwisho wa wimbo wao wa pamoja, Arrow alimgeukia Nadia huku akiambia hadhira kwamba bado ana hisia za mapenzi kwake, umati ukaanza kufoka maneno ya kumhimiza apige magoti aombe msamaha.
Mwanzo alisusia akisema kwamba alishaweka goti chini mbele ya Nadia wakati wa kumchumbia lakini mashabiki hawakukubali lakini mwishowe alipiga magoti akisema, “Kama nimekosa, kama sijui, kama nilivuka mipaka fulani, naomba unisamehe.”
Nadia hata hivyo alimkatiza na kumkumbusha waziwazi kwamba aliwahi kumtaja kuwa “side chick” wake kabla hajawa mpenzi wake rasmi, kauli iliyozua ukosoaji mkali ilipoibuka wakati wa kutengana kwao hadharani.
Msanii huyo mama wa watoto wawili hakukubali msamaha huo moja kwa moja akisema sio msamaha na labda hata Arrow Boy tayari ashapata mwingine na kuendeleza maisha yake.
Mchana leo, Arrow Boy alichapisha picha ya tukio hilo la kuomba msamaha na kumpongeza mke wake kwa onyesho lililofana na kwa muda ambao amekaa kwenye tasnia, hakusema lolote kuhusu iwapo alisamehewa.