Nyota wa muziki nchini Tanzania, Zuchu na Diamond Platnumz wamekaribisha mtoto wao wa kwanza pamoja ambaye ni wa kike, tukio lililoleta furaha kubwa kwa mashabiki wao ndani na nje ya Afrika Mashariki.
Wawili hao, ambao uhusiano wao umeangaziwa sana katika ulimwengu wa burudani, wanaripotiwa kusherehekea kuzaliwa salama kwa binti yao baada ya siku kadhaa za kusubiri kwa hamu.
Wote walichapisha picha wakiwa ndani ya chumba cha hospitali na binti yao ambaye wamemfunika, na kuandika, “Karibu duniani, malaika wetu mdogo wa thamani. Tayari unapendwa kuliko maneno yanavyoweza kueleza!”
Chini ya chapisho hilo linaloonekana kwenye akaunti za wote Zuchu aliandika, “Ulimwengu wangu wote”.
Habari za kujifungua kwa Zuchu zilijiri muda mfupi baada ya msanii huyo kuchapisha video akijiandaa kuelekea hospitalini, akionyesha furaha na wasiwasi wa kawaida kabla ya kujifungua.
Kabla ya hapo, wawili hao walikuwa pamoja kwenye sherehe ya kifahari ya kukaribisha mtoto na kufichua jinsia, iliyohudhuriwa na ndugu, marafiki na wasanii mbalimbali.
Katika hafla hiyo Diamond akimzawadi Zuchu Dola elfu 30 kama ishara ya upendo na shukrani.
Tangu taarifa hizo kuibuka, mitandao ya kijamii imefurika jumbe za pongezi kutoka kwa mashabiki, watu maarufu na wadau wa burudani wakimkaribisha mwanachama mpya wa familia ya Wasafi.
Hata hivyo, wawili hao bado hawajatoa taarifa rasmi zenye maelezo ya kina kuhusu mtoto wao mchanga, kama vile jina lake, huku wafuasi wao wakiendelea kuwatakia mema.