Mahakama Kuu nchini Kenya imekataa ombi la kundi la Rastafari la kutaka matumizi ya bangi kuhalalishwa kwa madhumuni ya kidini.
Jamii ya Rastafari ilikuwa imewasilisha kesi kortini ikidai kuwa marufuku ya matumizi ya bangi inakiuka haki yao ya uhuru wa dini na imani zinazolindwa na Katiba ya Kenya.
Katika uamuzi wake wa kihistoria, Jaji Bahati Mwamuye alisema kuwa jamii ya Rastafari haikuthibitisha kuwa sheria za kudhibiti dawa za kulevya zinakiuka haki zao za kikatiba.
Hata hivyo, alisisitiza kuwa kuna haja ya kuwa na mjadala mpana wa kitaifa kuhusu matumizi ya bangi.
Katika kesi yao, Chama cha Rastafari nchini Kenya kilidai kuwa bangi ni sakramenti takatifu katika dini yao na kiliomba waumini waruhusiwe kuikuza, kuimiliki na kuitumia kwa faragha wakati wa ibada bila hofu ya kukamatwa.
Warastafari walisisitiza kuwa matumizi ya bangi ni sehemu ya mafundisho ya dini yao na yanapaswa kuheshimiwa na kulindwa.
Hata hivyo, serikali ilipinga ombi hilo, ikisema kuwa kutoa msamaha wa kidini kungevuruga utekelezaji wa sheria za kupambana na dawa za kulevya na kufungua mianya ya biashara haramu ya bangi.
Jaji Mwamuye pia alisema ushahidi uliowasilishwa kuhusu nafasi ya bangi katika imani ya Rastafari hautoshi kuthibitisha kuwa matumizi yake ni sehemu muhimu ya dini hiyo.
Aliidhinisha uhalali wa kikatiba wa sheria zinazopiga marufuku kilimo, umiliki na matumizi ya bangi, hatua iliyokuwa pigo kubwa kwa mapambano ya kisheria ya Warastafari yaliyodumu kwa miaka sita.
Jaji huyo alisema kuwa ruhusa yoyote ya matumizi ya bangi kwa madhumuni ya kidini lazima iwe na msingi thabiti wa kikatiba na kisheria.