Maafisa zaidi ya 1,000 watumwa Ol Kalou kuhakikisha usalama

Martin Mwanje
2 Min Read
Inspekta Mkuu wa Polisi Douglas Kanja wakati akiwahutubia wanahabari Julai 14, 2026

Inspekta Mkuu wa Polisi Douglas Kanja amewahakikishia wakazi wa Ol Kalou usalama wa kutosha wakati wa uchaguzi mdogo ulioratibiwa kufanyika Alhamisi wiki hii. 

Kanja amesema maafisa zaidi ya 1,000 wametumwa eneo hilo kuhakikisha usalama unadumishwa wakati wa uchaguzi huo hususan katika vituo vyote 114 vya kupigia kura.

“Hii ina maana kwamba tuna maafisa wa polisi zaidi ya wawili kwa kila kituo cha kupigia kura. Kazi yao itakuwa kulinda karatasi za kupigia kura, mchakato wenyewe wa kupiga kura wakati wakitoa usalama wa kutosha katika kila kituo cha kupigia kura,” alisema Kanja wakati akiwahutubia wanahabari leo Jumanne, siku moja kabla upigaji kura kuandaliwa Ol Kalou.

“Zaidi yao, kuna timu maalum ambazo zimetumwa ili kuhakikisha hakuna ukiukaji wa usalama utatokea kama ifuatavyo; nimetuma kikosi cha maafisa wanne wa GSU, nimetuma kikosi cha maafisa wanne wa kupambana na wizi wa mifugo, na pia nimepeleka mizinga minne ya maji.”

Hatua hiyo inachukuliwa wakati ambapo visa vya vurugu vimeshuhudiwa katika eneo bunge la Ol Kalou wakati wa kipindi cha kampeni kilichomalizika rasmi jana Jumatatu kwa mujibu wa sheria.

Sheria inahitaji kampeni kumalizika saa 48 kabla ya kura kupigwa.

Uchaguzi mdogo wa Ol Kalou umeibuka kuwa wenye ushindani mkali hasa kati ya chama tawala cha UDA na kile cha upinzani cha DCP.

Muchina Nyagah anapeperusha bendera ya UDA kwenye uchaguzi huo huku Sammy Waweru akipeperusha ile ya DCP.

Uchaguzi mdogo wa Ol Kalou unaandaliwa kufuatia kifo cha aliyekuwa mjumbe wa eneo hilo David Njuguna Kiaraho mapema mwaka huu.

 

Share This Article