Rais Ruto akaribisha Starlets Ikulu

Hatua hiyo ililenga kusherehekea ufanisi wa timu hizo baada ya kufuzu kushiriki mashindano ya kimataifa.

Marion Bosire
2 Min Read

Rais William Ruto leo Jumanne amekuwa mwenyeji wa timu za kitaifa za wanawake za soka Harambee Starlets na Junior Starlets katika Ikulu ya Nairobi.

Hatua ya kiongozi wa nchi ililenga kusherehekea ufanisi wa timu hizo baada ya kufuzu kushiriki mashindano ya kimataifa.

Harambee Starlets imefuzu kushiriki mashindano ya mwaka huu ya kombe la mataifa ya Afrika la wanawake WAFCON nchini Morocco Julai 25 hadi Agosti 16 2026.

Harambee Junior Starlets kwa upande mwingine imefuzi kushiriki Kombe la Dunia la FIFA la Wanawake walio chini ya umri wa miaka 17 nchini Morocco vile vile, Oktoba 17 hadi Novemba 7, 2026.

Rais aliisifu Junior Starlets kwa mafanikio ya kihistoria, akibainisha kuwa imefuzu kwa mashindano hayo kwa mara ya pili katika historia ya Kenya baada ya kuishinda Afrika Kusini katika mechi muhimu ya kufuzu iliyochezwa katika Uwanja wa Kitaifa wa Nyayo.

Alimpongeza Kocha Mildred Cheche na wataalamu wengine kwa kuiongoza timu hiyo kufikia kushiriki Kombe la Dunia kwa mara ya pili, na kuwahimiza wachezaji kulenga zaidi ya hatua ya makundi katika mashindano hayo.

Ruto alisema uwekezaji wa Kenya katika maendeleo ya michezo, ikiwemo mipango ya kukuza vipaji mashinani na kuboresha miundombinu, ulilenga kulea mabingwa wa siku zijazo.

Rais pia aliipongeza Harambee Starlets kwa kufuzu kwa WAFCON 2026, akisema timu zote mbili zinawakilisha azma inayokua ya Kenya katika soka.

Share This Article