Sifuna aondolewa rasmi kama Katibu Mkuu wa ODM

ORPP iliafikia uamuzi huo baada ya kudurusu nyaraka za ODM na kubaini kuwa Sifuna hakuwasilisha majibu kama inavyotakiwa.

Marion Bosire
2 Min Read

Afisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, ORPP imemwondoa rasmi Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna kutoka kwenye orodha ya viongozi wa Chama cha Orange Democratic Movement (ODM) kama Katibu Mkuu.

Hatua hii sasa inakomesha miezi kadhaa ya mvutano kuhusu wadhifa wake.

Katika barua aliyotumiwa Sifuna kwa afisi yake bungeni jana Alhamisi, msajili alisema uamuzi huo ulifikiwa baada ya kudurusu nyaraka zilizowasilishwa na ODM na kubaini kuwa Sifuna hakuwasilisha majibu kama inavyotakiwa chini ya Kifungu cha 47 cha Katiba.

Msajili alisema kuondolewa kwa Sifuna kulifanyika kwa kuzingatia Sheria ya Vyama vya Siasa pamoja na Katiba ya ODM, na kuongeza kuwa rekodi rasmi za chama tayari zimeboreshwa ili kuonyesha mabadiliko hayo.

Kupitia kwa wakili wake Isaac Okero, Sifuna alipinga uamuzi huo akidai kuwa Msajili aliharakisha mchakato na hakufuata taratibu zilizowekwa chini ya Kifungu cha 20(2) cha Sheria ya Vyama vya Siasa.

Okero alisema watachukua hatua stahiki za kisheria kupinga uamuzi huo.

Akizungumza katika makao makuu ya ODM jijini Nairobi, Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho ambaye pia ni Mbunge wa kaunti ya Busia, Catherine Omanyo, alikaribisha uamuzi wa Msajili akisema utawezesha chama kusonga mbele.

Alimtuhumu Sifuna kwa kuendesha ajenda yake binafsi na kusema ODM sasa inaweza kupanga upya uongozi wake bila migogoro ya ndani.

Share This Article