Maafisa wa polisi katika kaunti ndogo ya Tseikuru, kaunti ya Kitui, wamepata mbuzi 22 waliokuwa wameibwa kutoka Kijiji cha Nzitu.
Baada ya kupokea habari kuhusu kuibwa kwa mifugo hao, maafisa wa usalama walianzisha operesheni mara moja kuwasaka wezi hao, ambao walitoroka baada ya kufumaniwa na polisi.
Kulingana na Huduma ya Taifa ya Polisi, mifugo wote waliokuwa wameibwa walipatikana na wanazuiliwa wakisubiri kukabidhiwa wenyewe, huku uchunguzi ukiendelea kuwatafuta wahusika wa wizi huo.
Wakati huo huo, hali ya utulivu imerejea katika eneo hilo baada ya mashambulizi baina ya jamii yaliyosababisha vifo vya watu 7 na wengine kadhaa kichwa na majeraha.
Kikosi cha maafisa wa polisi kutoka kitengo cha GSU, na polisi wa kawaida, walipelekwa kuzuia mashambulizi zaidi katika mipaka ya Kitui–Tana River na Kitui–Garissa.
Gavana wa Kitui Julius Malombe, amewahimiza wakazi kushirikiana Kwa karibu ma maafisa wa usalama kurejesha utulivu na amani huku hali hiyo ikiendelea kushughulikiwa.
Gavana huyo alihakikisha kuwa serikali ya kaunti ya Kitui inatoa msaada wa kibinadamu na kiakili kwa waathiriwa wa mashambulizi hayo.