Kesi ya kusikiliza kubanduliwa kwa Gachagua imeahirishwa

Tom Mathinji
1 Min Read

Kesi ya kusikiliza kubanduliwa afisini kwa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, imeahirishwa hadi Mei 7, 2026.

Kesi hiyo iliyokuwa imeratibiwa kuanza Jumatatu hadi Jumatano Juma hili, imeahirishwa ili kutoa fursa kwa Jaji Antony Mrima kushiriki mahojiano kama mmoja wa jopo la uteuzi wa Tume ya kuwaajiri watumishi wa Idara ya Mahakama (JSC).

Siku ya Jumatatu katika Mahakama Kuu ya Milimani, Gachagua alishikilia kuwa mchakato uliotumika kumuondoa mamlakani haukuzingatia Sheria.

Kundi lake la mawakili likiongozwa na Wakili Mkuu Paul Muite, lilisema kuwa mchakato uliotumika kumuondoa Gachagua afisini, ulikiuka katiba na ulimnyima haki yake ya kujitetea.

Muite aliongeza kuwa mchakato huo uliharakishwa bila kuzingatia usawa.

Naibu huyo Rais wa zamani aliondolewa mamlakani  Oktoba  17, 2024, baada ya Maseneta kuthibitisha mashtaka 11 yaliyolimbikiziwa dhidi yake.

Share This Article