Waziri wa Usalama wa Taifa Kipchumba Murkomen, amewahakikishia wananchi kwamba uchunguzi wa kina umeanzishwa kuhusiana na mkasa wa moto uliotokea katika shule ya wasichana ya Utumishi kaunti ya Nakuru.
Akizungumza alipowatembelea wanafunzi waliojeruhiwa wanaoendelea kupokea matibabu katika hospitali ya St. Joseph Gilgil, Murkomen alisema wale watakaopatikana na hatia watawajibishwa.
“Tutafanya kila tuwezalo kuhakikisha kama kuna yeyote aliyehusika na kuzuka kwa moto huo, wanachukuliwa hatua ili haki ipatikane kwa waliofariki na wale waliojeruhiwa,” alisema Murkomen.
Waziri huyo aliwatakia afueni ya haraka wanafunzi waliojeruhiwa, wakati huo huo akitoa wito kwa Wakenya kuombea jamii nzima ya shule hiyo.
Takriban wanafunzi 16 walifariki na wengine zaidi ya 70 kujeruhiwa baada ya moto kuzuka katika shule hiyo usiku wa kuamkia Alhamisi, chanzo chake kikisalia kuwa kitendawili.
Waziri wa elimu Julius Ogamba ameagiza shule hiyo ifungwe mara moja.