Wanafunzi 6 wa Utumishi Academy kupokea matibabu maalum KNH

Awali, Waziri wa Elimu Julius Ogamba alitangaza kuwa wanafunzi 7 wamelazwa hospitalini kutokana na majeraha waliopata.

Martin Mwanje
2 Min Read
Mmoja wa wanafunzi waliojeruhiwa katika mkasa wa moto alipotembelewa na Mawaziri Julius Ogamba na Kipchumba Murkomen

Wanafunzi wawili wa shule ya Utumishi Girls Academy iliyopo mjini Gilgil, kaunti ya Nakuru wamesafirishwa hadi Hospitali ya Kitaifa ya Rufaa ya Kenyatta, KNH kwa matibabu maalum. 

Wanafunzi wengine 4 wanatarajiwa kusafirishwa hadi kwenye hospitali hiyo ili kutibiwa baada ya kupata majeraha kutokana na mkasa wa moto uliotokea katika shule hiyo usiku wa kuamkia leo.

Awali, Waziri wa Elimu Julius Ogamba alisema wanafunzi 7 kati ya 79 waliojeruhiwa walikuwa wamelazwa hospitalini wakiendelea kupokea matibabu.

Wanafunzi 71 walitibiwa na kuruhusiwa kwenda nyumbani huku mmoja akichukuliwa na mzazi wake.

Ripoti zinaashiria maafisa wa ngazi ya juu serikalini wakiongozwa na Waziri wa Usalama wa Taifa Kipchumba Murkomen wanatarajiwa kuwatembelea wanafunzi hao KNH ili kuwaombea dua na kuwatakia nafuu ya haraka.

Murkomen amewahakikishia Wakenya kwamba uchunguzi madhubuti utafanywa ili kubaini chanzo cha moto huo.

“Tutafanya kila tuwezalo ili kuhakikisha ikiwa kuna yeyote aliyehusika katika moto huu, haki inatendeka, ili maisha ya waliofariki na majeraha waliopata wenzenu yawajibiwa,” aliahidi Murkomen.

Wanafunzi kadhaa wa shule hiyo walihojiwa kuhusiana na janga hilo.

Awali, Waziri Ogamba alitangaza kufungwa kwa shule ya Utumishi Girls Academy kufuatia mkasa huo uliotokea saa 6:15 usiku.

Lengo ni kupisha, miongoni mwa mambo mengine, upelelezi wa kilichosababisha moto huo na kuruhusu kutolewa kwa ushauri nasaha kwa wanafunzi na wazazi walioathiriwa wakati maombolezi ya wanafunzi 16 waliofariki yakiendelea.

Jumla ya wanafunzi 200 walikuwa kwenye bweni wakati mkasa huo ulipotokea.

 

 

 

 

Share This Article