Zuchu na Marioo wang’ara kwenye tuzo za TMA

Marion Bosire
2 Min Read

Tuzo za TMA ziliandaliwa usiku wa Oktoba 19 2024 ambapo Zuchu aliibuka mwanamuziki bora wa kike huku Marioo akishinda tuzo sawia kwa upande wa wanaume.

Diamond Platnumz alijishindia tuzo ya wimbo bora wa densi pamoja na ile ya mtumbuizaji bora huku Christian Bella akishinda tuzo ya msanii bora wa muziki wa densi.

Leila Rashid mke wake mwimbaji Mzee Yusuf aliibuka mshindi katika kitengo cha wimbo bora wa taarab, huku Akili Mali akishinda tuzo ya msanii bora wa muziki wa Reggae wa mwaka.

Tuzo ya wimbo bora wa reggae wa mwaka iliwaendea Warriors from East kupitia wimbo “Wewe” na tuzo ya msanii bora wa mwaka wa Dancehall ikachukuliwa na Baddest 47.

Tuzo ya wimbo bora wa Dancehall wa mwaka ilimwendea Mr. Hater wa Appy.

Harmonize kwa upande mwingine aling’aa katika kitengo cha albamu bora ya mwaka kupitia albamu kwa jina “Visit Bongo” na akang’aa tena kwenye kitengo cha wimbo bora wa mwaka kupitia kibao “Single Again”.

Dulla Makabila alituzwa msanii bora wa muziki wa singeli aliyokuwa aking’ang’ania pamoja na D Voice, Lamona, Dogo Elisha na Mchina Mweusi.

Tuzo ya msanii bora chipukizi ilimwendea Chino huku S2Kizzy akishinda tuzo ya mwandalizi bora wa muziki.

Hafla ya kutoa tuzo hizo iliandaliwa katika ukumbi wa Super Dome, Masaki, jijini Dar es Salaam nchini Tanzania.

Share This Article