Kansiime kuwachukulia hatua waliochapisha video za onyesho lake

Hii ni baada ya mtu kurekodi video ya onyesho lake la vichekesho na kuichapisha mitandaoni bila idhini.

Marion Bosire
2 Min Read

Mchekeshaji wa Uganda Anne Kansiime ametishia kuwachukulia hatua waliorekodi video za tukio lake na kuzichapisha mitandaoni bila idhini yake.

Akizungumza siku moja baada ya onyesho hilo la vichekesho aina ya ‘Roast’ Anne aliyekuwa nyumbani alishangaa jinsi mtu anaingia kwenye tukio la mtu anarekodi video na kuzichapisha kama maudhui yake.

Msanii huyo alilalamika akisema kwamba alitumia pesa nyingi kuandaa tukio hilo na kulirekodi kisha mwingine atumie kamera mbovu na kuchapisha video hiyo kwenye mtandao wa YouTube.

“Mtu anakuja kwenye onyesho langu, anarekodi video na kuichapisha kwenye akaunti yake kama kazi yake binafsi. Jamani nilidhani tumepita nyakati kama hizi.” alisema Anne kwenye video aliyochapisha kwenye TikTok.

Aliendelea kushangaa jinsi mtu huyo alichapisha kazi yake bila idhini kama njia ya kumzuia yeye mmiliki wa kazi hiyo kujipatia mapato kutokana na kazi hiyo.

“Na unafikiria sitakuchukulia hatua?” aliuliza Kansiime akimlenga mtu huyo ambaye hakumtaja.

Kansiime aliandaa onyesho la kwanza la vichekesho vya kejeli vilivyomlenga yeye, onyesho alilolipa jina la “The Kansiime Comedy Grill”.

Onyesho hilo la Kansiime lilikomesha pia uvumi uliosambaa awali kwamba yeye na mchumba wake ambaye pia ni baba ya mtoto wake Skylanta walikuwa wameachana.

Sasa imebainika kwamba matendo ya wawili hao mitandaoni yalilenga kutangaza kazi ya muziki ya Skylanta aliyokuwa ametoa, wimbo ambao ulihadithia kuhusu mpenzi wa zamani.

Website |  + posts
Share This Article