Washukiwa watatu wa ujambazi wamekamatwa katika kile ambacho maafisa wa upelelezi DCI wanakitaja kuwa kukomeshwa mara moja kwa ujambazi.
Kelvin Baraza Andayi au Kevoo, Titus Mutuku Maingi au Tush na Jack Wilshere Kimathi au Jack sasa wako kizuizini kufuatia oparesheni kabambe ya maafisa wa polisi.
Watatu hao walikamatwa baada ya uchunguzi wa kina uliowahusisha na kisa cha wizi wa kimabavu katika kampuni ya Sanergy EPZ huko Kinanie, eneo la Athi-River, Februari 23, 2025.
Siku hiyo washukiwa hao na wengine wawili ambao bado hawajakamatwa walijihami na kuvamiakampuni hiyo ambapo waliteka wafanyakazi na kuwadhulumu.
Baadaye waliondoka na bidhaa mbali mbali kama jokofu, choko, betri mbili za lori, mbili za trekta na mtambo jenereta wakitumia gari aina ya pickup.
Maafisa wa upelelezi wa eneo la Athi River walianzisha uchunguzi mara moja huku wakitumia ushahidi uliowaelekeza kwa nyumba moja ya kupangisha katika eneo la Kamulu, ambapo kiongozi wa genge hilo Kelvin Baraza Andayi alipatikana na kukamatwa.
Upekuzi wa nyumba yake ulipelekea kupatikana kwa bastola moja aina ya Beretta, simu, sare za polisi, kadi sita za simu na vitu vingine.
Andayi alielekeza maafisa hao hadi eneo la Gimu huko Athi-River, ambako washukiwa wenza Maingi na Kimathi walipatikana na kukamatwa pia.
Wanaandaliwa kwa ajili ya kufikishwa mahakamani huku maafisa wa upelelezi wakifuatilia taarifa zaidi ili kupata washukiwa wengine. Bidhaa zilizopatikana zimechukuliwa kwa ajili ya kutumika kama ithibati katika uchunguzi.