Wanafunzi kusoma kwa awamu Thika kufuatia uhaba wa madarasa

Martin Mwanje
2 Min Read

Uhaba wa madarasa mjini Thika, kaunti ya Kiambu huenda ukasababisha wanafunzi wa shule za upili kusoma kwa awamu.

Washikadau wa elimu mjini humo wamependekeza kuwepo kwa awamu mbili ya masomo kwenye shule za eneo hilo kwa sababu ya idadi kubwa ya wanafunzi.

Wakiongozwa na mjumbe wa Thika Mjini Alice Ng’ang’a wakati wa hafla ya kuwatuza wanafunzi wa shule ya upili ya wasichana ya Chania walionawiri katika mtihani wa KCSE mwaka jana, wadau hao walisema kuwa, wanafunzi wa shule za kutwa, watagawanywa kwa makundi mawili. Kundi la kwanza litasoma kutoka usubuhi hadi mchana nalo la pili kutoka mchana hadi jioni.

Changamoto hii imetajwa kutokana na mpango wa serikali wa kuwataka wanafunzi wote waliofanya mtihani wa KCPE kujiunga na shule za upili.

Kwa mujibu wao, shule nyingi za eneo hilo zina zaidi ya wanafunzi 1,000 huku darasa moja likiwa na wanafunzi 100 na hivyo kuwalemea walimu.

Kwa upande wake, Ng’ang’a aliunga mkono kauli hiyo na kusema kuwa itasaidia wakati huu ambao ujenzi wa madaras zadi unaendelea.

Mwalimu Mkuu wa shule ya upili ya wasichana wa Chania Mary Mwangi, alielezea jinsi shule hiyo imeathirika kwani kwa miaka mitatu iliyopita, wanafunzi wa madarasa saba kati ya tisa ya kidato cha kwanza wamesomea kwa hema.

Mwaka jana, mbunge Ng’ang’a kwa ushirikiano na washikadau wengine, alibadilisha shule ya msingi ya Jamhuri kuwa ya upili kwa ajili ya kukimu idadi hii kubwa ya wanafunzi. Kwa sasa, shule hiyo ina wanafunzi 220.

Mbunge huyo vile vile analenga kujenga shule nyingine ya kutwa kwenye wadi ya Kamenu.

TAGGED:
Share This Article