Kilio cha wahudumu wa baharini Kwale

Marion Bosire
1 Min Read

Wahudumu wa baharini wakiwemo wavuvi katika eneo la shimoni huko lungalunga kaunti ya kwale, wanamtaka Rais Wiliam Ruto kumrejesha kazini aliyekuwa Waziri wa Madini na Uchumi Samawati Salim Mvurya.

Kulingana na wahudumu hao, Mvurya alileta mabadiliko makubwa katika sekta ya uvuvi na madini nchini na ingekuwa bora iwapo angerejeshwa kazini.

Wakiongozwa na Omari Mtengo, Katibu wa Vitengo vya Uvuvi Pwani, wahudumu hao wamesema kuwa kuteuliwa kwa Mvurya awali kulileta mabadiliko makubwa katika sekta ya madini, uvuvi na uchumi samawati nchini, sekta ambayo ilikuwa imedorora kabla ya kuteuliwa kwake.

Kufufuliwa kwa vikundi vya usimamizi wa baharini (Bmus) katika eneo la pwani, utoaji wa maboti ya kisasa ya uvuvi pwani na kutolewa kwa ruzuku kwa makundi ya wavuvi nchini ili kujiendeleza kimaisha ni miongoni mwa mafanikio ya Mvurya wakati akihudumu kama waziri.

Himizo sasa linatolewa kwa Rais Ruto kumjumuisha Mvurya katika Baraza la Mawaziri ambalo bado anaunda baada ya kuvunja lile la awali.

Rais Ruto yuko mbioni kuunda Baraza Jipya la Mawaziri na tayari ameteua mawaziri 11 ambao watasailiwa na bunge kabla ya kuidhinishwa rasmi. Aliahidi kutangaza mawaziri wa nyadhifa zilizosalia katika muda wa siku chache zijazo.

Website |  + posts
Share This Article