Kamati ya Bunge la Senate kuhusu Habari, Mawasiliano na Teknolojia (ICT), imetambua kwamba wakazi wa kaunti ya Kilifi wanakabiliwa na changamoto ya kupata huduma za serikali.
Kwenye ziara yake katika Makao Makuu ya Kaunti ya Kilifi, Kamati hiyo ilibaini kuwa kuna kituo kimoja cha Huduma Center kinacho wahudumia wakazi kutoka wakilishi wadi 35.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo Allan Chesang ambaye ni Seneta wa Trans Nzoia, alidokeza kuwa kamati hiyo imepokea malalamishi kuhusu upatikanaji wa huduma za serikali katika kaunti hiyo, hususan idadi ndogo ya vituo vya Huduma Center.
Wakiwa katika kituo hicho cha huduma center, Maseneta hao walikagua huduma mbalimbali zinazotolewa na serikali, utumizi wa majukwaa ya mtandao katika utoaji huduma na changamoto zinazowakabili wananchi katika upatikanaji wa huduma hizo.
Aidha, ukosefu wa nguvu za umeme mara kwa mara, pia umetajwa kuwa swala linalohujumu utoaji huduma na ucheleweshaji wa mchakato wa usajili na utoaji vitambulisho vya taifa.
Naibu mwenyekiti wa kamati hiyo Miraj Abdillahi, alielezea wasiwasi kutokana na idadi kubwa ya vijana ambao hawana vitambulisho vya taifa, hatua inayowasababisha kukosa huduma na miradi muhimu ya serikali.
Alidokeza kuwa, ukosefu huo wa vitambulisho vya taifa, unahujumu usajili kwenye Halmashauri ya Afya ya Jamii (SHA), mradi wa nyumba za gharama nafuu, na fursa za ufadhili kwa wanaunzi walio katika vyuo vikuu.
Ziara hiyo ni sehemu ya mpango wa Senate Mashinani initiative, unaotoa fursa kwa Bunge la Senate kushirikiana kwa karibu na wakazi na kutambua changamoto zinazowakabili wananchi katika upatikanaji wa huduma za serikali.