Wakazi Dar es Salaam waagizwa kuwa na mapipa ya takataka

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, nchini Tanzania, Albert Chalamila, alikiri Jiji hilo ni chafu, akisema Viongozi walijisahau kwa muda katika suala la usafi.

Marion Bosire
2 Min Read
Albert Chalamila, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Tanzania.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, nchini Tanzania, Albert Chalamila, ameagiza kila nyumba kuwa na mapipa au vifaa vya kuhifadhi takataka angalau viwili.

Alisema hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha Jiji la Dar es Salaam linakuwa safi na mazingira yanatunzwa.

Akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari leo Septemba 17, 2026, Chalamila amesema hatua hiyo itasaidia kutekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, la kuhakikisha Dar es Salaam inakuwa safi.

Amesema pamoja na nyumba, magari ya abiria maarufu kama daladala yanapaswa pia kuwa na vifaa maalumu vya kuhifadhi taka ili kuzuia uchafu kutupwa ovyo.

Katika mkutano huo, Chalamila vile vile alikiri kwamba Jiji hilo ni chafu, akisema Viongozi walijisahau kwa muda katika suala la usafi.

Chalamila alizungumzia hatua zinazochukuliwa kuhakikisha Jiji hilo linakuwa safi na salama wakati mamlaka zikijiandaa kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua inayotarajiwa katika msimu wa mwaka huu.

Chalamila amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali, Taasisi zinazohusika na usafi wa mazingira na Wananchi katika kuhakikisha taka hazizuii mifereji na njia za kupitisha maji Jijini.

“Tulisahau kwa muda, jambo ambalo limepelekea Mheshimiwa Rais kwa jicho lake kuona Dar es salaam ni chafu, tunakiri kwamba Rais alichokiona kwetu hajatuonea,” amesema Chalamila.

Share This Article