Ujumbe wa Minnesota wajadili ushirikiano na KMTC

Ujumbe huo unaongozwa na Mwakilishi wa Jimbo la Minnesota katika Wilaya ya 38A, Huldah Momanyi-Hiltsley, wa asili ya Kenya.

Marion Bosire
1 Min Read

Wauguzi waliohitimu nchini Kenya huenda hivi karibuni wakapata fursa za ajira nchini Marekani kufuatia mazungumzo ya ushirikiano kati ya Taasisi ya Mafunzo ya Tiba ya Kenya, KMTC na ujumbe kutoka jimbo la Minnesota.

Ujumbe huo, ukiongozwa na Mwakilishi wa Jimbo la Minnesota katika Wilaya ya 38A, Huldah Momanyi-Hiltsley, wa asili ya Kenya, ulizuru makao makuu ya KMTC jijini Nairobi kujadili fursa za ushirikiano katika mafunzo ya uuguzi, uajiri na upatikanaji wa ajira kimataifa.

Wakati wa ziara hiyo, wajumbe hao kutoka sekta ya afya nchini Marekani walitembelea Idara ya Uuguzi na vituo vya mafunzo vya KMTC.

Walikutana pia na wahadhiri pamoja na wanafunzi, na kujadili masuala ya mafunzo ya kitaaluma, ukuzaji wa ujuzi na njia za kupata ajira.

Ushirikiano unaopendekezwa unalenga kukabiliana na uhaba wa wauguzi katika vituo vya afya vya Minnesota huku ukifungua fursa za ajira za kimataifa kwa wauguzi wa Kenya waliohitimu.

Hata hivyo, wauguzi watakaotaka kunufaika na fursa hizo watahitajika kutimiza masharti ya leseni za kitaaluma na uhamiaji kabla ya kuajiriwa nchini Marekani.

Share This Article