Shirika la Msalaba Mwekundu tawi la Kenya, limesema linaendelea kuwapokea raia wa Ethiopia wanaoingia Kenya, wakitoroka mapigano kwenye mpaka wa Moyale.
“Katika eneo la Moyale, maafisa wetu wanaendelea kuhudumia familia zinazowasili Kenya kufuatia ukosefu wa usalama mpakani,” lilisema shirika hilo kwenye ukarasa wa X.
Kulingana na shirika hilo, baadhi ya misaada ya kibinadamu inayotolewa ni pamoja na makazi ya muda, hema, blanketi na vyombo vingine vya nyumbani.
Aidha, raia hao wa Ethiopia pia wanapewa chakula na huduma ya kwanza, huku shirika hilo likiendelea kukadiria hali ilivyo kwa ushirikiano na serikali ya kaunti ya Marsabit na washirika wengine kutoa msaada kwa waathiriwa hao.
Mamia ya raia wa Ethiopia, wengi wao wakiwa wanawake, watoto na vijana, wamevuka kuingia nchini Kenya tangu mapigano kuzuka siku ya Jumatano.