Msanii wa muziki wa hip-hop nchini Uganda, Tom Mayanja, maarufu kama The Mith, anatarajiwa kusherehekea safari yake ya muziki na utambulisho wa kitamaduni wa Uganda.
Atafanya hivyo kupitia tamasha itakayofanyika Jumamosi, Novemba 14, katika uwanja wa Kati-Kati, jijini Kampala.
Tamasha hiyo iliyopatiwa jina la “THE SO UG EXPERIENCE” kaulimbiu ikiwa “A Flight to Uganda”, itaangazia mchango wake katika kukuza muziki wa hip-hop nchini Uganda na muziki wa kitamaduni wa taifa hilo.
The Mith alianza safari yake ya muziki mwaka 1999 akiwa mwanachama wa kundi la Klear Kut, pamoja na Navio, Papito na Abba Lang.
Kundi hilo lilipata umaarufu kupitia albamu yake ya kwanza, “Mind, Body and Soul”, iliyokuwa na wimbo maarufu “All I Wanna Know” aliomshirikisha Juliana Kanyomozi.
Baadaye, The Mith alijijengea jina kama msanii huru kupitia miradi mbalimbali kama “Destination Africa” na “The Week of September”.
Albamu yake ya mwaka 2025 iitwayo “THE UGANDAN Vol. 2: BALI-OKWABWE”, ilishinda tuzo ya Albamu Bora katika tuzo za Hip Hop za mwaka 2025 nchini Uganda. Mwaka 2026, aliungana tena na Navio kutoa albamu ya pamoja “GODLVL”.
Tamasha hiyo itawajumuisha pia Navio, Lilian Mbabazi, Maurice Kirya, Winnie Nwagi, Elijah Kitaka, Feffe, BigTril na Flex D’Paper.
Uganda Waragi inafadhili tamasha hiyo kupitia kampeni yake ya SO UG inayolenga kuenzi ubunifu, utamaduni na utambulisho wa Uganda.