Kenya yaanza safari ya kutokomeza Ebola kabisa

Waziri wa Afya, Aden Duale, ametangaza siku 42 za kuhesabu kuelekea kutangazwa kwa Kenya kuwa isiyo na Ebola kuanzia Alhamisi, Novemba 12, 2026.

Marion Bosire
2 Min Read

Kenya imeanza rasmi safari ya kuelekea kutangazwa kuwa haina ugonjwa wa Ebola baada ya kumruhusu mgonjwa wa mwisho kutoka hospitalini.

Watu wengine 11 waliokuwa wakifuatiliwa nao wameachiliwa huru, baada ya kukamilisha siku 21 za uangalizi bila kuonyesha dalili za ugonjwa huo.

Waziri wa Afya, Aden Duale, ametangaza kuwa siku 42 za kuhesabu kuelekea kutangazwa kwa Kenya kuwa isiyo na Ebola zitaanza Alhamisi, Novemba 12, 2026.

Nchi hii inatarajiwa kupata hadhi hiyo kufikia Desemba 23, iwapo hakutakuwa na maambukizi mapya.

Akizungumza katika afisi za wizara ya afya leo Jumatano, Novemba 11, Duale alisema watu wote 135 waliokuwa wametagusana na mgonjwa wa kwanza aliyeingiza ugonjwa huo nchini, walifuatiliwa kwa mafanikio.

Alibainisha kuwa visa vyote tisa vilivyothibitishwa vilitokana na mkondo mmoja wa maambukizi, bila ushahidi wa ugonjwa huo kusambaa katika jamii.

Wizara ya Afya itaendelea kuimarisha ufuatiliaji na ukaguzi katika maeneo ya kuingilia nchini na kuweka wahudumu wa kukabiliana na dharura katika hali ya tahadhari.

Duale amehakikishia Wakenya na wageni kwamba nchi iko wazi kwa biashara, utalii, usafiri na safari, bila vikwazo vya kutembea au mikusanyiko ya umma.

Aliwataka watakaopata dalili za Ebola, hasa baada ya kusafiri katika maeneo yaliyoathiriwa, kutafuta matibabu mara moja au kupiga simu ya bure 719.

Waziri huyo pia ameahidi uwazi na uwajibikaji katika matumizi ya rasilimali zilizopokelewa kukabiliana na Ebola nchini.

Share This Article