Serikali imeazimia kuimarisha operesheni za kiusalama na juhudi za kuleta amani, kwenye mpaka kati ya Isiolo na Garissa kufuatia machafuko ya kijamii yaliyosababisha maafa na uharibifu wa mali.
Hatua hiyo ya serikali inajiri baada ya mkutano ulioandaliwa na Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen na viongozi wa kaunti hizo mbili, kukadiria hali ya usalama na hatua za kurejesha utulivu.
Kulingana na taarifa ya wizara hiyo, Inspekta Jenerali wa Polisi ameagizwa kutekeleza operesheni ya kijasusi ili kutwaa silaha haramu katika kaunti hizo mbili.
“Huduma ya Taifa ya Polisi itatathmini uwezo wa maafisa wa polisi wa ziada (NPR), kutoa mafunzo upya kwa maafisa hao, na kuwaondoa maafisa wanaotumia vibaya silaha zao,” ilisema taarifa hiyo..
Aidha, taarifa hiyo ilidokeza kuwa uchukuzi wa maafisa wa polisi utaimarishwa, huku kaunti hizo mbili zikipewa kipaumbele kwenye ununuzi wa magari ya polisi.
Maswala mengine yatakayozingatiwa ni kubuni kamati za amani, mikakati ya utumiaji wa rasilimali kwa pamoja, na kushirikiana na kampuni za mawasiliano kuimarisha upatikanaji wa intaneti.
Hata hivyo, serikali ilisema itaharakisha ujenzi wa barabara za kiusalama katika maeneo yaliyoathiriwa.