Makumbusho ya Raila Odinga: Winnie ahimiza utulivu wa kisiasa

Anawakata wanasiasa kutoka mirengo yote kuweka kando tofauti zao za kisiasa na kuruhusu hafla ijayo kuwa makumbusho ya utulivu.

Marion Bosire
2 Min Read

Winnie Odinga bintiye Hayati Raila Amolo Odinga, amehimiza utulivu wa kisiasa huku mipango ikiendelea ya hafla ya kumkumbuka babake, Oktoba 15, 2026.

Winnie ambaye anawakilisha Kenya katika bunge la Afrika Mashariki alikuwa akizungumza katika hafla ya kuipokeza familia yao nyumba ya kaburi la babake nyumbani kwao Opoda Farm.

Anawakata wanasiasa kutoka mirengo yote kuweka kando tofauti zao za kisiasa na kuruhusu hafla ijayo kuwa makumbusho ya utulivu.

Winnie alisema wageni watakaohudhuria kumbukumbu hiyo hawapaswi kulazimishwa kuachana na misimamo yao ya kisiasa, akisisitiza kuwa urithi wa Raila ulijengwa juu ya uwezo wa kukubali mitazamo tofauti.

“Tunaweza kuwa na misimamo tofauti ya kisiasa, tunaweza kutofautiana vikali kuhusu mwelekeo wa kisiasa wa nchi yetu, lakini mnakaribishwa hapa. Hakuna anayehitajika kuacha imani yake mlangoni,” alisema.

Alilinganisha hilo na uhusiano wa Raila na aliyekuwa Rais Daniel arap Moi, akikumbuka jinsi wawili hao hatimaye walipatana baada ya miaka kadhaa ya migogoro ya kisiasa na Raila kuzuiliwa wakati wa utawala wa Moi.

Kwa Winnie, maridhiano hayo yalionyesha uwezo wa babake kutenganisha tofauti za kisiasa na mahusiano binafsi, na kuacha nyuma chuki za zamani.

Alikumbuka Raila alivyohudhuria kumbukumbu ya Moi, ambapo alitambua mateso aliyopitia wakati wa kuzuiliwa, lakini pia akatangaza kuwa wawili hao walikuwa wamepatana.

Alisema historia hiyo inapaswa kuongoza maadhimisho ya Oktoba 15, huku ushindani wa kisiasa ukizidi kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027.

Winnie pia aliwataka watakaohudhuria kumbukumbu hiyo kulinda uhuru wa kidemokrasia ambao Raila aliendeleza kwa miongo kadhaa, ikiwemo haki ya kutoa maoni tofauti bila hofu ya kuteswa.

Alirejelea maneno yaliyoandikwa kwenye kaburi la Raila, “Demokrasia ni gharama ya uhuru,” kama ukumbusho wa kafara zilizotolewa katika harakati za kupigania uhuru wa kisiasa.

“Demokrasia ikilinda uhuru wetu, na tuiweke katika vitendo hata pale sauti tunayosikia inapopinga misimamo yetu,” alisema.

Share This Article