Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, DPP ameidhinisha mashtaka dhidi ya aliyekuwa Katibu katika Wizara ya Michezo, Balozi Peter Kirimi Kaberia, maafisa wengine wanne wa serikali na wafanyabiashara watano.
Kumi hao wanadaiwa kufuja shilingi milioni 330, pesa za umma.
Fedha hizo zilikuwa zimetengwa kwa ajili ya maandalizi ya Kenya kuwa mwenyeji wa Mashindano ya Mataifa ya Afrika, CHAN, mwaka 2018.
Kulingana na taarifa ya Ofisi ya DPP, hatua hiyo imefuatia uchunguzi uliofanywa na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi Nchini, EACC, ambayo iliwasilisha faili ya uchunguzi kwa DPP kwa ajili ya mapitio.
Baada ya kutathmini ushahidi kwa kina na kwa njia huru, DPP ilisema imebaini msingi wa kutosha wa kuwafungulia mashtaka washukiwa hao pamoja na kampuni zilizohusishwa.
Mbali na Kaberia, watakaoshtakiwa ni Stephen Njoroge Muthuma, Harun Chebet Komen, Enock Ondwari Onditi na John Kiende Ruga.
Wafanyabiashara waliotajwa ni Marcos Gonzalez Puente, Samuel Mbai Njoroge, Kitheka Muema, Anthony Mwangi Kimanthi na Ephraim Kinyua Muchangi.
Kampuni sita pia zimehusishwa katika kesi hiyo.
Mashtaka yanayowakabili ni pamoja na matumizi mabaya ya ofisi, ununuzi haramu wa mali ya umma, kutofuata sheria za manunuzi, kupokea mapato ya uhalifu na utovu wa nidhamu wa kifedha.