Ruto asema sarafu ya Kenya imeimarika pakubwa

Alisema pia kwamba akiba ya fedha za kigeni iliongezeka kutoka dola bilioni 7.37 mwaka 2022 hadi dola bilioni 15.3 mwaka huu.

Marion Bosire
2 Min Read

Rais William Ruto ametangaza kwamba sarafu ya Kenya imeimarika pakubwa na mfumuko wa bei umepungua, akitaja hatua hizo kama ishara ya kuimarika kwa uchumi wa taifa licha ya changamoto zinazoendelea za gharama ya maisha.

Akizungumza wakati wa hotuba yake ya Hali ya Taifa bungeni leo Novemba 18, 2026, Ruto alisema shilingi imekuwa ikibadilishwa kwa wastani wa shilingi 129 dhidi ya dola moja ya Marekani, ikilinganishwa na karibu KSh162 mwaka 2022.

Alisema mfumuko wa bei, uliokuwa wa kiwango cha asilimia 9.6 mwaka 2022, ulipungua hadi wastani wa asilimia 4.1 mwaka 2025, ingawa kupanda kwa gharama za chakula na nishati kulisababisha ongezeko jingine mwezi Oktoba mwaka huu.

Ruto pia alisema akiba ya fedha za kigeni iliongezeka kutoka dola bilioni 7.37 mwaka 2022 hadi kufikia kilele cha dola bilioni 15.3 mwaka huu.

Kuhusu gharama ya maisha, alitaja hatua za kupunguza bei ya mbolea kutoka shilingi 7,500 hadi 2,000 kwa gunia la kilo 50, akisema ongezeko la uzalishaji wa mahindi limechangia kushuka kwa bei ya unga wa kilo mbili hadi wastani wa 152 mwezi Septemba 2026.

Hata hivyo, alikiri kuwa gharama za chakula na nishati bado zinaendelea kuwa changamoto, akiahidi kuwa serikali itaendelea kutekeleza mikakati ya kufanya bidhaa na huduma muhimu ziwe nafuu zaidi kwa wananchi.

Share This Article