Muungano wa Kitaifa wa Wauguzi na Wakunga wa Kenya, KNUNM umeapa kuendelea na mgomo wa wauguzi kote nchini hadi wiki yake ya tano.
Wauguzi wanasisitiza kwamba mgomo huo utafika kikomo baada ya serikali na Baraza la Magavana kukubaliana kusaini na kutekeleza Mkataba wa Makubaliano ya Pamoja.
Muungano huo pia umeomba Rais William Ruto aingilie kati kufuatia madai ya kushambuliwa kwa wauguzi katika maandamano yaliyofanyika Kisii.
Mwenyekiti wa Kitaifa wa KNUNM, Joseph Gwosi, alisema mazungumzo yalikuwa yametatua suala la wauguzi waliokuwa wakifanya kazi kwa mikataba chini ya mpango wa Huduma ya Afya kwa Wote, UHC, huku wafanyakazi walioathirika wakianza kupokea barua zinazothibitisha kuajiriwa kwao kwa masharti ya kudumu.
Alisema muungano huo na Baraza la Magavana pia wamekubaliana kuunda kamati ya pamoja itakayoshughulikia uundaji wa miongozo ya maendeleo ya taaluma kwa wauguzi.
Hata hivyo, Gwosi alisema utekelezaji wa mkataba wa makubaliano ya pamoja, bado ndio suala kuu ambalo halijatatuliwa.
“Suala ambalo hatujakubaliana ni jambo moja ambalo ni muhimu sana kwa wauguzi. Nalo ni suala la mkataba wa ajira, ambao kwa Kiingereza unajulikana kama CBA. Hapo tunataka kuliambia taifa na wahudumu wetu wa afya ambao ni wauguzi kwamba hatuna makubaliano na serikali,” alisema.
Muungano huo unakadiria kwamba utekelezaji wa makubaliano hayo, utagharimu takribani shilingi bilioni 5.9 kiasi ambacho Gwosi alisema serikali inaweza kumudu.