Kinara wa chama cha ODM Dkt. Oburu Oginga amekanusha madai ya kulazwa hospitalini wakati hali yake ya kiafya ikisuasua.
Kinyume cha madai hayo yaliyochapishwa na baadhi ya vyombo vya habari mitandaoni, Dkt. Oginga anasema yu buheri wa afya na hakuna sababu ya kuhofu.
“Nilitembelea tu hospitali kwa muda mfupi ili madaktari wangu wanifanyie uchunguzi wa jumla na tayari nimerejea nyumbani,” alisema Dkt. Oginga kwenye taarifa fupi.
“Kuwa mgonjwa ni kitu cha kawaida na hakipaswi kumtia hofu yeyote. Siku ambayo hakika nitakuwa mgonjwa, nitawafahamisha nyote, kwani mimi ni mtu mwenye uwazi mno.”
Dkt. Oginga, mwenye umri wa miaka 82, alichukua hatamu za kukiongoza chama cha ODM baada ya kifo cha kaka yake Raila Odinga mwaka jana.
Raila alikumbana na mauti wakati akitibiwa katika hospitali moja nchini India.
Alifariki akiwa na umri wa miaka 80.