Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, tayari amewasili katika uwanja wa Mwehe, huko Makunduchi, Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar, kwa ajili ya kushiriki Kilele cha Tamasha la Kizimkazi 2026.
Jana usiku Rais Samia alihudhuria tamasha ya burudani ambayo ni sehemu ya tamasha kuu ya Kizimkazi ambapo alifurahia burudani kutoka kwa wasanii mbali mbali kama Nandy, Jose Chameleone, Ali Kiba na Harmonize.
Jana mchana kiongozi huyo wa Tanzania aliweka jiwe la msingi na kupanda mti katika shule ya Sekondari ya Ufundi Kizimkazi Mkunguni, Wilaya ya Kusini, Mkoa wa Kusini Unguja.
Hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa miradi ya Muungano, ukiwemo ujenzi wa skuli hiyo unaotekelezwa na Mamlaka ya Elimu Tanzania, TEA, kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, WEMA.
Akihutubia wahudhuriaji wa Usiku wa Kizimkazi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, alisema Tamasha ya Kizimkazi imeendelea kuwa jukwaa la kutangaza fursa za uwekezaji na maendeleo katika eneo la Kizimkazi na Mkoa wote wa Kusini Unguja.