Rais William Ruto leo Jumatano atahutubia taifa kutoka majengo ya bunge katika kikao cha pamoja kitakachowaleta pamoja wabunge wa Bunge la Taifa na Maseneta.
Hii itakuwa ni mara ya nne kwa Rais Ruto kuhutubia taifa tangu alipoingia madarakani mwaka 2022.
Rais Ruto anatarajiwa katika majengo ya bunge majira ya 8 na kuanza kuhutubia taifa majira ya saa tisa alasiri baada ya kukagua gwaride la heshima.
Kwenye hotuba yake, Rais Ruto ataangazia hatua zilizopigwa na serikali yake katika kutimiza ahadi za kabla ya uchaguzi mkuu.
Masuala ya miundombinu kama vile ujenzi wa nyumba za gharama nafuu, upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta, JKIA na ujenzi wa barabara ya Rironi-Mau Summit yanatarajiwa kuangaziwa.
Katika sekta ya afya, Ruto pia anatarajiwa kumulika ufanisi ulioafikiwa katika utekelezaji wa Mamlaka ya Afya ya Jamii, SHA na mapambano yanayoendelea dhidi ya ugonjwa wa Ebola ambao umesababisha vifo vya watu wawili hadi kufikia sasa.
Katika sekta ya elimu, kiongozi wa taifa pia anatarajiwa kuangazia mafanikio yaliyopatikana ikiwa ni pamoja na kuajiri walimu 100,000 wakati wengine 20,000 wakitarajiwa kuajiriwa mwezi ujao.
Naibu Rais Kithure Kindiki, Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi, Mawaziri na Mabalozi wa nchi mbalimbali ni miongoni mwa viongozi wanaotarajiwa kuhudhuria kikao hicho.