Ageng’o: Serikali itahakikisha haki za watoto zinalindwa

Ageng'o aliyasema hayo alipofanya ziara ya kutathmini taasisi kadhaa za ulinzi wa watoto katika kaunti za Busia na Kakamega.

Tom Mathinji
1 Min Read
Carren Ageng’o - Katibu wa Huduma za Watoto.

Katibu wa Huduma za Watoto Carren Ageng’o, amesema serikali itachukua hatua madhubuti kulinda haki za watoto, na kuimarisha ulinzi wa watoto kote nchini.

“Kuimarishwa kwa mifumo ya ulinzi wa watoto, kunahitaji uangalizi endelevu, ushirikiano dhabiti, na taasisi imara kuhakikisha kila mtoto anatunzwa, analindwa na anapata usaidizi anaohitaji,” alisema Katibu Ageng’o.

Ageng’o aliyasema hayo alipofanya ziara ya kutathmini taasisi kadhaa za ulinzi wa watoto katika kaunti za Busia na Kakamega.

Katika kaunti ya Busia, katibu huyo na ujumbe wake walizuru afisi ya kaunti inayoshughulikia watoto, kabla ya kuzuru kitengo cha kuwashughulikia watoto katika Makao Makuu ya Polisi ya Kaunti hiyo na kujadiliana na maafisa wa polisi katika kitengo hicho.

Alisema ziara hiyo imetoa fursa ya kutathmini utendakazi wa mikakati ya ulinzi wa watoto, katika semhemu ambapo watoto wanatangamana na mfumo wa utekelezaji sheria na haki.

Akiwa Kakamega, katibu huyo na ujumbe wake walikagua ujenzi wa mradi wa shule ya watoto ya  kurekebishia tabia na jela ya watoto ya Kakamega.

Alikuwa ameandamana na Mshirikishi wa maswala ya watoto eneo la Magharibi mwa nchi Esther Wasige, pamoja na maafisa wengine kutoka idara ya huduma za watoto.

Share This Article