Afisa wa polisi akamatwa Kibera kwa madai ya kula rushwa

Martin Mwanje
1 Min Read
Mshukiwa wa upokeaji rushwa, Carrey Odhiambo Ongeng

Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi, EACC imemkamata konstebo wa polisi Carrey Odhiambo Ongeng kwa madai ya kuitisha na kupokea hongo ya shilingi 50,000. 

Ongeng anahudumu katika Ofisi ya Idara ya Upelelezi wa Jinai, DCI mtaani Kibera.

Afisa huyo anadaiwa kuitisha pesa hizo kutoka kwa mkazi wa Kibera kama sharti la kuripoti malalamiko ya ulaghai katika Kitabu cha Matukio (OB) na kuanzisha uchunguzi.

EACC inasema baada ya kupokea malalakiko, wapelelezi wake walianzisha operesheni kali katika kituo cha polisi cha Kibera alikokamatwa afisa huyo wakati akidaiwa kupokea pesa hizo.

Mshukiwa alipelekwa katika makao makuu ya EACC huko Integrity Centre kuandikisha taarifa na kisha kuachiliwa kwa dhamana ya shilingi 50,000 pesa taslimu akisubiri kufanywa kwa uchunguzi zaidi.

Tume hiyo imeahidi kuimarisha vita dhidi ya uitishaji hongo na kutoa wito kwa umma kuwa mstari wa mbele kupiga ripoti wanapoitishwa hongo katika jitihada zao za kutafuta huduma.

 

Share This Article