Tume ya Maadili na Kukabiliana na Ufisadi (EACC), imeanzisha mchakato wa kuwatambua wawaniaji wa nyadhifa za kisiasa wanaokabiliwa na maswala ya kimaadili na ufisadi kabla ya Uchaguzi Mkuu mwaka 2027.
Akizungumza Jijini Nairobi, Afika Mkuu Mtendaji wa EACC Abdi Mohammud, alisema tume hiyo inabuni orodha ya majina ya walio na maswala ya kimaadili na itawasilisha majina hayo kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kabla ya Uchaguzi Mkuu.
Mohamud alisema wapigaji kura wana jukumu la pamoja la kuwachagua viongozi wanaoweza kulinda rasilimali za umma, akidokeza kwamba uongozi unaozingatia maadili ni muhimu katika kukuza uwajibikaji na kuimarisha taasisi za umma.
kwa upande wake, mwenyekiti wa EACC David Oginde, alisema Wakenya wana jukumu la kuwachagua viongozi walio na viwango vya juu vya maadili.
Huku akiwashtumu baadhi ya viongozi wakuu wa kisiasa kwa kutumia matamshi ya uchochezi yanayoweza kuvuruga amani nchini, Oginde alisema EACC inafuatilia kwa karibu wanasiasa wanaotumia lugha za matusi na kuchochea uhasama wa kisiasa hapa nchini.
Mkutano huo ulioandaliwa chini ya kaulimbiu “Kuongoza kwa uadilifu katika nyakati ngumu: Njia ya kuafiki Amani na ustawi,” ulilenga kuimarisha uadilifu katika taasisi za umma na kukuza uongozi wenye uwajibikaji.