Kenya imethibitisha kisa kimoja cha ugonjwa wa Ebola unaosababishwa na virusi vya Bundibugyo.
Ugonjwa huo mekuwa mwiba katika Jamhuri ya Demokrasia ya Congo, DRC na nchi jirani ya Uganda.
Nchini DRC pekee, watu zaidi ya 4,000 wamethibitishwa kufariki kutokana na ugonjwa huo.
Akitangaza kuthibitishwa kwa kisa cha kwanza cha Ebola nchini Kenya leo Jumanne, Waziri wa Afya Aden Duale amesema mwathiriwa wa ugonjwa huo tayari amefariki.
“Mgonjwa ambaye ni raia wa Kenya, ambaye aliyeishi nchini DRC kwa kipindi cha miaka 7, aliugua takriban mwezi mmoja uliopita na alitibiwa katika hospitali kadhaa wakati akiwa bado yupo DRC,” alisema Duale.
“Alisafiri kutoka DRC hadi Kampala kwa kutumia barabara na kisha kuabiri ndege ya Jambo Jet nambari ya usajili 8523 na kuwasili jijini Nairobi Jumamosi, Oktoba 3, 2023 saa 7:10 mchana.”
Kulingana na Waziri Duale, mgonjwa huyo alifanyiwa ukaguzi wa kawaida wa afya punde baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa JKIA kabla ya kusafirishwa moja kwa moja hadi hospitali moja jijini Nairobi kwenye gari aina ya Toyota Fielder nambari ya usajili KDG 699Z alikotengwa.
Kisha alionyesha dalili kama vile homa, uchovu mwingi na kudhoofika, koo kuwasha na maumivu ya misuli miongoni mwa dalili zingine.
Ni dalili zilizosababisha mgonjwa huyo kufanyiwa uchunguzi wa kina na kisha kubainika kuwa aliambukizwa ugonjwa wa Ebola.
“Mgonjwa huyo alipatiwa usaidizi wa matibabu lakini kwa bahati mbaya, alifariki jana usiku,” aliongeza Duale wakati akituma risala za rambirambi kwa familia na marafiki wa marehemu.
Mazishi ya mwenda zake yamepangwa kufanyika leo Jumanne kwa mujibu wa taratibu za usalama zilizowekwa za kudhibiti ugonjwa wa Ebola.
Watu 28 waliotangamana na marehemu tayari wametambuliwa, wakiwemo wahudumu wa afya na jamaa wa marehemu, ambao sasa watawekwa kwenye karantini.