Wenyeji Marekani ndio timu ya 10 kufuzu kwa raundi ya 16 ya Kombe la Dunia baada ya kuwalemea Bosnia Herzegonia mabao 2-0 mapema leo Alhamisi ugani San Francisco.
Florian Balogun aliwaweka Marekani uongozini katika dakika 45 baada ya bao la awali kukataliwa kwa kuotea.
Balogun alipigwa kadi nyekundu katika dakika ya 64 kwa kucheza ngware na kuwalazimu wenyeji kucheza wakiwa 10 uwanjani kwa takriban dakika 30.
Zikisalia dakika nane kipenga cha mwisho kipulizwe, Malik Tillman alipata mwanya kupitia shambulizi la kushtukiza na kupachika goli wakati Bosnia walikuwa wamejituma mbele kutafuta bao la kusawazisha.
Marekani sasa watamenyana na Ubelgiji Jumanne ijayo, Julai 7 katika awamu ya 16 bora uwanjani Seattle.