Azimio yaazimia kufanya mabadiliko kuelekea 2027

Muungano huo umeamua kufanyia mabadiliko uongozi wa ndani ili kunoa makali yake kabla ya kuandaliwa kwa uchaguzi mkuu mwakani.

Tom Mathinji
2 Min Read
Azimio yafanya mabadiliko kabla ya Uchaguzi Mkuu 2027.

Muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya Coalition umetangaza kutekeleza mabadiliko wakati unapojiandaa kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.

Mabadiliko hayo yaliidhinishwa kwenye mkutano wa pamoja wa Baraza Kuu na Kamati Tekelezi ya Kitaifa ya muungano huo.

Ni mkutano  ulioongozwa na kinara wa chama cha Wiper Stephen Kalonzo Musyoka, huku maamuzi ya mkutano huo yakitangazwa na Katibu Mkuu Caroli Omondi ambaye pia ni mbunge wa Suba Kusini.

Kulingana na Omondi, mkutano huo uliamua kufanyia mabadiliko uongozi wa ndani wa muungano huo ili kuimarish kabla ya uchaguzi mkuu mwakani.

“Baraza hilo liliamua kubadilisha muundo wa muungano, vitengo kadhaa vya muungano pamoja na kuunda upya muungano wa Azimio Coalition,” alisema Omondi.

Kama sehemu ya mfumo mpya, muungano huo umewakaribisha Mawaziri wa zamani Fred Matiang’i wa Usalama na Peter Munya wa Kilimo, na Seneta wa zamani wa Embu Lenny Kivuti kwa baraza la uongozi wake kwa lengo la kuboresha utoaji maamuzi.

Aidha, mkutano huo pia ulikubali kupanua muungano huo kwa kukikaribisha chama cha Democratic Action Party-Kenya (DAP-K), kinachoongozwa na Eugene Wamalwa, kujiuga nao tena kuambatana na taratibu za uidhinishaji zilizopo.

Vyama vingine vilivyokaribishwa kujiunga na Azimio ni kile cha Umoja na Maendeleo Party kinachoongozwa na aliyekuwa Gavana wa Meru Kawira Mwagaza, People’s Democratic Party (PDP) kinachoongozwa na Omingo Magara, na chama cha Democratic Party (DP), kinachoongozwa na Spika wa zamani wa Bunge la Taifa Justin Muturi.

Hata hivyo, mkutano huo ulimtwika Kalonzo jukumu la kushirikisha vyama vingine vya kisiasa vilivyo na maono sawa kubuni muungano wa upinzani kabla ya uchaguzi mkuu.

Miongoni mwa vyama vinavyolengwa ni pamoja na Democracy for Citizens Party (DCP) kinachoongozwa na Naibu Rais wa zamani Rigathi Gachagua, People’s Liberation Party (PLP) kinachoongozwa na Martha Karua, United Green Movement na Linda Mwananchi Movement punde usajili wake utakapokamilika.

Share This Article