Mmoja wa polisi wa Kenya waliotumwa kudumisha amani nchini Haiti amefariki.
Polisi huyo alifariki jana Jumapili baada ya kujeruhiwa wakati wa operesheni ya usalama katika taifa hilo la Caribbean linalohangaishwa na magenge ya wahalifu.
Kenya imetuma maafisa wa polisi zaidi ya 900 nchini Haiti ambao ni sehemu ya kikosi cha kimataifa cha kudumisha amani nchini humo (MSS).
Kifo cha polisi huyo wa Kenya kimethibitishwa na Kamanda wa Kikosi cha MSS Godfrey Otunge.
“Leo, Jumapili, Februari 23, 2025, mmoja wa maafisa wetu wa MSS kutoka kikosi cha Kenya alijeruhiwa wakati wa operesheni katika eneo la SÉGUR – SAVIEN, katika idara ya Artibonite. Afisa huyo alisafirishwa kwa ndege mara moja hadi hospitali ya Aspen Level 2 lakini kwa bahati mbaya, alifariki kutokana na majeraha aliyopata,” alisema Otunge kwenye taarifa.
Wiki chache zilizopita, kundi la nne la polisi wa Kenya liliwasili nchini Haiti kwa misheni ya kulinda amani.
Polisi hao ambao walijiunga na MSS, waliondoka nchini mapema mwezi huu kwa operesheni hiyo.
Kundi hilo la nne la polisi wa Kenya kwenda nchini Haiti, liliwajumuisha wanawake 24 kati ya maafisa 144 wa usalama, kwa lengo la na kushirikiana na wenzao walio Haiti kudumisha usalama.
Polisi hao walipokelewa na maafisa wakuu wa serikali ya mpito nchini Haiti, akiwemo Rais Leslie Voltaire na Kamanda wa MSS Godfrey Otunge.