NCIC yamhoji mwanasiasa Trufosa Kutto

Alitoa matamshi ya chuki Oktoba 31, 2026, katika Kijiji cha Tambwo, Koloch Serem, Kaunti ya Nandi.

Marion Bosire
1 Min Read
Dkt. Kepha Omae - Mwenyekiti wa NCIC

Tume ya Uuwiano na Utangamano wa Kitaifa, NCIC imemhoji mwanasiasa Trufosa Jelagat Kutto kuhusu matamshi yanayodaiwa kuchochea mgawanyiko wa kijamii katika Kaunti ya Nandi.

Kutto alifika katika ofisi za tume hiyo zilizopo Britam Towers, Nairobi, jana Jumatatu, Novemba 9, 2026, kufuatia wito aliotumiwa Novemba 2.

Wito huo unahusiana na matamshi anayodaiwa kutoa Oktoba 31, 2026, katika Kijiji cha Tambwo, Koloch Serem, Kaunti ya Nandi.

Alifika mbele ya tume hiyo saa tano asubuhi akiwa ameandamana na wakili wake, na kujibu madai yaliyokuwa yakichunguzwa na kuwasilisha maelezo yake kupitia wakili wake.

Katika taarifa yake, Mwenyekiti wa NCIC, Askofu Dkt. Kepha Nyamweya Omae, alisema Kutto alipatiwa nafasi ya kujibu madai hayo na kutoa maelezo yake.

Tume hiyo sasa itapitia maelezo yake, ushahidi na taarifa nyingine muhimu kabla ya kutoa uamuzi wake.

NCIC imesisitiza kujitolea kwake kutekeleza majukumu yake kwa haki na bila upendeleo, huku ikiwataka viongozi na wananchi kujizuia kutoa matamshi yanayoweza kuhatarisha amani na umoja wa kitaifa.

Share This Article