Kushirikisha umma: Kutoka kanuni hadi utekelezaji

Naibu Jaji Mkuu Philomena Mwilu anasema Katiba ya mwaka 2010 iliweka mamlaka ya juu ya nchi mikononi mwa wananchi.

Marion Bosire
2 Min Read

Mahakama ya Upeo ya Kenya inaendelea kubadilisha ushirikishaji wa umma kutoka kuwa kanuni ya kikatiba na kuwa fundisho la kisheria linaloweza kutekelezwa, haya ni kulingana na Naibu Jaji Mkuu Philomena Mbete Mwilu.

Akizungumza katika taasisi ya sheria ya chuo kikuu cha Kenyatta huko Parklands katika hadhara ya Mahakama ya Upeo, Jaji Mwilu alisema Katiba ya mwaka 2010 ilibadilisha uhusiano kati ya wananchi na Serikali kwa kuweka mamlaka ya juu ya nchi mikononi mwa wananchi.

Mwilu alitaja maamuzi muhimu ya Mahakama ya Juu, ikiwemo kesi ya kampuni ya BAT Kenya, ambayo iliweka vigezo vya kushirikisha umma kwa njia ya maana kutoa taarifa kwa wakati unaofaa, ushirikishaji wa makundi mbalimbali, uwazi, kueleweka kwa mada inayojadiliwa na kutoa fursa halisi kwa wananchi kutoa maoni.

Jaji Mwilu pia alizungumzia uamuzi wa Mahakama kuhusu Sheria ya Fedha wa mwaka 2024, uliolenga kusawazisha ushirikishaji wa umma na muda uliowekwa kikatiba wa kutunga sheria.

Alisema marekebisho yanayotokana na maoni ya wananchi hayalazimishi moja kwa moja mchakato mpya wa ushirikishaji, lakini maoni ya umma lazima yachukuliwe kwa uzito.

Aidha, alitaja Mswada wa Ushirikishaji wa Umma wa mwaka 2025, ulioidhinishwa na Bunge la Taifa tarehe 12 Agosti 2026, kama hatua kuelekea kuweka mfumo mmoja wa ushirikishaji wa umma katika taasisi za serikali.

Akihimiza mawakili vijana kukumbatia ushiriki wa kiraia kupitia teknolojia ya kidijitali, Jaji Mwilu alisema Katiba iliweka kanuni hiyo, mahakama zikaiendeleza kuwa fundisho la kisheria, lakini wananchi na taasisi ndio watakaobeba jukumu la kuamua mustakabali wake.

“Utekelezaji wake na mustakabali wake bado ni jukumu letu sote,” alisema.

Share This Article