Kiwanda cha kusafisha mafuta chazinduliwa Lamu

Rais Ruto ameeleza mradi huo kuwa hatua kubwa katika kuimarisha usalama wa nishati na kukuza viwanda Afrika Mashariki.

Marion Bosire
2 Min Read

Kenya imezindua ujenzi wa mradi wa kiwanda cha kusafisha mafuta na kemikali za petroli cha thamani ya shilingi Trilioni 2, katika kaunti ya Lamu.

Rais William Ruto ameeleza kuwa mradi huo ni hatua kubwa katika kuimarisha usalama wa nishati na kukuza viwanda katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Akizungumza katika hafla ya kuweka jiwe la msingi huko Mokowe leo Jumatano, Septemba 30, 2026, Ruto alisema Kiwanda cha Kusafisha Mafuta cha Dangote Afrika Mashariki kitakuwa na uwezo wa kusindika hadi mapipa 700,000 ya mafuta ghafi kwa siku na kuzalisha hadi megawati 1,000 za umeme.

Rais alisema mradi huo utasaidia Kenya na nchi jirani kupunguza utegemezi wa bidhaa za petroli zilizosafishwa kutoka nje, huku ukifungua fursa za uzalishaji wa bidhaa nchini na kuongeza thamani ya malighafi.

Kwa mujibu wa Ruto, Kenya ilitumia takriban shilingi bilioni 530 kuagiza bidhaa za petroli mwaka uliopita, akiamini kwamba kusafisha mafuta karibu na masoko ya kikanda kunaweza kusaidia kukidhi mahitaji ya nishati ya nchi.

Mradi huo unatarajiwa kuwa kichocheo cha maendeleo yanayozunguka Bandari ya Lamu na mradi wa LAPSSET, huku serikali ikikadiria kuwa unaweza kuzalisha ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja zipatazo 60,000.

Ruto pia aliahidi kuwepo kwa ulinzi wa maslahi ya jamii za eneo hilo, ikiwa ni pamoja na kushughulikia masuala ya ardhi kwa haki, kulinda mazingira na kutoa fursa kwa wakazi na wafanyabiashara wa Lamu.

Alisema serikali itashirikiana na Dangote pamoja na mamlaka za eneo hilo kuhakikisha fursa za mafunzo, ajira na zabuni zinawanufaisha Wakenya.

Share This Article