Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka, IEBC, imeongheza maandalizi ya kuhakikisha usalama wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.
IEBC inatoa wito wa ushirikiano wa karibu miongoni mwa wadau wa usalama, haki na wadau wengineo ili kuzuia vurugu na kulinda haki za wapiga kura na wagombea.
Mwenyekiti wa tume hiyo Erastus Ethekon amesisitiza dhamira yao ya uhuru, uwazi na uaminifu katika utendaji kazi wao kuelekea uchaguzi huo.
Akizungumza wakati wa mkutano wa Mpango wa Maandalizi ya Usalama wa Uchaguzi (ESAP) jijini Mombasa, Ethekon alisema hakuna Mkenya kamwe anapaswa kuhofia kushiriki uchaguzi.
Ametoa wito kwa wadau kuimarisha ushirikiano kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.

Mpango huo unawaleta pamoja IEBC, Huduma ya Taifa ya Polisi, taasisi za upelelezi na mashtaka, taasisi za uangalizi na washikadau wengine.
Lengo ni kufanya tathmini ya pamoja ya hatari, kuimarisha mifumo ya maonyo ya mapema, kuratibu miitikio na kuhakikisha uchunguzi wa kuaminika kuhusiana na makosa ya uchaguzi.
Taarifa ya KNA