Afisa Mkuu wa ushirikishaji wa wananchi na huduma kwa wateja katika serikali ya Kaunti ya Nairobi, Geoffrey Mosiria, ametangaza nia yake ya kuwania ugavana Nairobi.
Katika taarifa aliyochapisha kwenye mitandao ya kijamii, Mosiria alisema amesikiliza wito wa wakazi wa Nairobi wanaomtaka awanie wadhifa huo wa juu katika kaunti hiyo.
Mosiria alitaja uzoefu wake katika utumishi wa umma akisema umemwandaa kwa majukumu makubwa zaidi.
Mosiria alimpongeza mkuu wake wa sasa kwa kumpa fursa za kuhudumu, akisema ametekeleza majukumu aliyopewa licha ya kuhamishwa kutoka idara moja hadi nyingine.
Alidai kuwa utendakazi wake umemwezesha kutambuliwa na umma, akiongeza kuwa wakazi wanaamini wadhifa wake wa sasa ni mdogo ikilinganishwa na kiwango cha huduma wanachotarajia kutoka kwake.
“Niko tayari kuhudumu. Niko tayari kuirekebisha Nairobi,” alisema Mosiria, akitumia kaulimbiu za “Bwana wa Kutatua Matatizo” na “Bwana wa Umakini Zaidi” kuelezea azma yake ya kuwania ugavana.
Alifichua pia kwamba ameshauriana na watu mbalimbali, akiwemo kiongozi wa chama cha Jubilee, Fred Matiang’i, aliyesema yuko tayari kuandamana naye katika safari ya kuboresha Nairobi na kuchangia maendeleo ya Kenya.
Mosiria alisema viongozi watakaotafuta mamlaka mapya mwaka 2027 hatimaye watahukumiwa na wapiga kura, akisisitiza kuwa wakazi wa Nairobi ndio wataamua anayestahili fursa nyingine ya kuwahudumia.