Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi Eliud Lagat, amezindua kitengo cha polisi cha kukabiliana na dharura (QRU), chenye makao yake Garissa.
Kitengo hicho ambacho kina wanachama 229, kimejukumiwa kukabiliana na ugaidi ,wizi wa mifugo na migogoro baina ya jamii katika eneo nzima la kaskazini mashariki mwa nchi na nchi Jirani.
Akiongea wakati wa hafla ya uzinduzi wa kitengo hicho Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi Eliud Lagat, alimtawaza kamishna wa polisi Samuel Mukuusi kuwa Kamanda wa kwanza wa kitengo hicho.
“Tumekuja Garissa leo kuzindua kitengo cha Quick Response Unit (QRU), ambacho kinakuja kushughulikia maswala ya kiusalama katika maeneo kadhaa ya nchi hususan Garissa, Isiolo, Laikipia, Samburu na Mandera,” alisema Lagat.
Lagat aliagiza kitengo hicho kushirikiana kwa karibu na vitengo vingine vya kiusalama, kuziba mianya ya utekelezaji inayotumiwa na magenge ya uhalifu
Huku wakiahidi usaidizi endelevu wa vifaa vya kisasa na mafunzo Lagat alitoa changamoto kwa Kamanda wa kitengo hicho Mukuusi kudumisha nidhami,uwajibikaji na kuheshimu haki za kibinadamu,akiwakumbusha maafiaa kuwa oparesheni kali ya kimkakati lazima itekelezwe kwa kuzingatia sheria.
“Hatua hi itaboresha hali ya usalama katika mipaka ya Garissa na Isiolo, ambako kumekuwa na ghasia za kijamii zilizosababisha maafa,” aliongeza Lagat.