Wakili Ndegwa Njiru atakiwa kufika mbele ya NCIC

Njiru anatarajiwa kufika mbele ya tume hiyo Alhamisi tarehe tatu Disemba, 2026 saa tano asuhubi kuhusiana na matamshi hayo aliyoyatoa Novemba 22.

Tom Mathinji
2 Min Read
Ndegwa Njiru - Wakili.

Tume ya Taifa ya Mshikamano na Utangamano (NCIC), imemtaka wakili Ndegwa Marclus Njiru kufika mbele yake kutokana na matamshi aliyotoa dhidi ya Rais William Ruto wakati wa mkutano wa kisiasa eneo la Mwala, kaunti ya Machakos.

Njiru anatarajiwa kufika mbele ya tume hiyo Alhamisi tarehe 3 Disemba, 2026 saa tano asuhubi kuhusiana na matamshi hayo aliyoyatoa Novemba 22.

Kwenye barua iliyomwandikia wakili huyo tarehe 26 November, tume hiyo ilisema uchunguzi wa awali umebaini kuwa kuna ukiukaji wa katiba, sheria za Mshikamano na Utangamano wa Kitaifa na kanuni za adhabu.

Baadhi ya matamshi anayodaiwa kutoa ni pamoja na kumuita Rais “takataka”, akimlaumu kwa kuwaua watu, kufanikisha ufisadi na kuuza kampuni ya Safariom.

“Huyu William Ruto ameua watoto wetu, huyu William Ruto ameleta ufisadi, huyu William Ruto ameiba mali yetu, ameuza Safaricom, amemaliza Kenya, aende asiende?” ilisema barua hiyo iliyoandikwa kwa Njiru.

Kulingana na NCIC, matamshi hayo yanaibua wasiwasi kuhusu kuvuruga amani na kuchochea uhasama wa kisiasa na kikabila.

Aidha, tume hiyo ilisema matamshi hayo yalielekezwa kwa rais ambaye sehemu ya 131(1) ya katiba inamtambua kuwa ishara ya umoja wa kitaifa.

NCIC pia inachunguza uwezekano wa kukiuka sehemu ya 28 na 33(3) ya katiba, ambazo zinaelezea kuhusu heshima ya kibinadamu, na uhuru wa kujieleza.

Tume hiyo imeonya kuwa iwapo wakili huyo atakosa kufika mbele yake, agizo la kukamatwa kwake litatolewa, au ashtakiwe kwa makosa ya uhalifu.

Share This Article