Za mwizi arobaini zatimia, polisi bandia anaswa Nairobi

Iliwabidi polisi kumkamata mwanamume huyo baada ya kudokezwa na raia waliomshuku kuwa askari bandia.

Dismas Otuke
1 Min Read

Maafisa wa polisi wa kituo cha Jogoo Road, kaunti ya Nairobi, wamemnasa mwanamume ambaye amekuwa akiwalaghai na kuhangaisha raia akijisingizia kuwa polisi.

Alipofumaniwa, mshukiwa huyo alijitambulisha kuwa Sajini Augustine Mjomba Mwadime na kudai kufanya kazi katika kituo cha mafunzo ya maafisa wa GSU mtaani Embakasi.

Polisi walipata cheti bandia cha kuajiriwa na nambari ya kufanya kazi ghushi, pingu mbili, funguo mbili na magwanda kadhaa ya polisi.

Pia maafisa wa polisi walimpata na vitambulisho bandia vya huduma ya kitaifa ya polisi.

Iliwabidi polisi kumkamata mwanamume huyo baada ya kudokezwa na raia waliokuwa wamemshuku kuwa askari bandia.

Share This Article